Shirika la habari la Ahlubayt (as)ABNA: Kiwango cha ushirikiano wa Iran na Qatar na hati za maelewano zitakazotiwa saini katika safari hii kinaweza kuwa kielelezo kikubwa cha uhusiano mzuri wa nchi hizi mbili jirani.
Kustawisha uhusiano na majirani na nchi za eneo la Magharibi mwa Asia na rafiki ni sehemu ya kipaumbele kikuu cha sera za nje cha serikali ya Rais wa Jamhuri ya Kiislamu ya Iran, Ebrahim Raisi. Kutokana na eneo lake la kijiografia, Iran inapakana na nchi 15, na hapana shaka kuwa kutumiwa vizuri uwezo wote wa kiuchumi, biashara, viwanda, utamaduni na utalii katika uhusiano na majirani na nchi za eneo hili, kutapelekea kustawishwa uhusiano wa pande mbili na wa pande kadhaa.
Qatar ni miongoni mwa nchi zinazolengwa na kupewa kipaumbele katika sera ya mambo ya nje za Iran, na historia ya uhusiano wa nchi hizi unaonyesha kuwa, Iran na Qatar zimekuwa na uhusiano mkubwa na unaozidi kukua na kustawi. Ziara ya Rais wa Jamhuri ya Kiislamu ya Iran nchini Qatar ni sehemu ya jitihada za Tehran za kupanua na kuimarisha uhusiano, na safari ya Qatar ni awamu ya kwanza ya ziara ya Rais wa Iran katika nchi za Kiarabu za Ghuba ya Uajemi; jambo ambalo linaonesha umuhimu maalumu wa uhusiano kati ya nchi hizo mbili.
Wakati baadhi ya nchi za Kiarabu, kwa kuungwa mkono na Marekani na wafuasi wake katika eneo la Asia Magharibi, zilipojaribu kutia doa na kuuharibu kabisa uhusiano wa Waarabu na Irani, Qatar iliendeleza uhusiano wake mzuri na Iran, na wakati huo huo ilifanya jitihada za kuhakikisha kwamba, mtazamo wa nchi za Kiarabu za kandokando ya Ghuba ya Uajemi unajiepusha na malengo ya Marekani na kuoana na hali halisi ya kanda hiyo.
Iran na Qatar daima zimekuwa zikiamini kuwa, njia pekee ya kutatua matatizo ya kieneo na hitilafu zilizopo ni ushirikiano, maelewano na maingiliano ya kujenga na ya kirafiki baina ya nchi za eneo hili zenyewe, na Tehran imekuwa ikifuata kanuni hiyo muhimu katika sera na vitendo vyake.
Katika ziara yake hiyo mjini Doha, Rais wa Jamhuri ya Kiislamu ya Iran atakutana na Sheikh Tamim bin Hamad Al Thani, Amir wa Qatar na kujadili uhusiano wa pande mbili, njia za kuimarisha uhusiano na masuala muhimu ya kieneo na kimataifa. Iran na Qatar zina fursa nzuri ya ushirikiano katika sekta mbalimbali za kisiasa, kiuchumi, kiviwanda, kibiashara, kifedha, baharini, utalii, fedha na nishati, na mazungumzo kati ya Rais wa Iran na Amir wa Qatar yanaweza kuandaa njia ya kupanua ushirikiano wa kina kati ya nchi hizo mbili na kuwa na matokeo mazuri kwa Tehran na Doha.
Ali Akbar Mehrabian, Waziri wa Nishati wa Iran amesema kuwa, mkataba wa maelewano utatiwa saini katika nyanja za kubadilishana umeme, kuunganisha mtandao wa umeme wa Iran na Qatar, biashara ya bidhaa, uwekezaji, kustawisha uhusiano kuhusu maeneo huru ya kibiashara, pamoja na utamaduni na utalii. Imetangazwa pia kwamba mikataba 4 katika sekta ya bahari na anga itatiwa saini kati ya nchi hizo mbili katika hafla itakayohudhuriwa na Rais wa Jamhuri ya Kiislamu ya Iran na Amir wa Qatar. Iran pia inashauriana na Qatar juu ya ujenzi wa njia ya chini ya bahari. Utekelezaji wa mradi huo wa kimkakati kati ya Iran na Qatar una umuhimu wa pekee na utaunganisha bandari ya Deir ya eneo la Bushehr kusini mwa Iran na nchi ya Qatar. Ujenzi wa njia hiyo ya baharini kati ya Iran na Qatar, mbali na kupanua ushirikiano wa baharini na bandari, utazidisha maendeleo ya sekta ya utalii kwa maslahi ya mataifa ya Iran na Qatar.
Safari ya Rais wa Jamhuri ya Kiislamu ya Iran nchini Qatar na mikataba muhimu ya pande mbili itafungua ukurasa mpya katika ujirani mwema, na Iran daima imekuwa ikitoa kipaumbele katika kupanuka uhusiano na majirani zake na nchi za eneo la Asia Magharibi katika siasa zake za nje.
Kwa msingi huo, kabla ya kuondoka mjini Tehran akielekea Doha mapema leo, Rais Sayyid Ebrahim Raisi amesema: Safari hii inafanyika kwa msingi wa kuimarisha mawasiliano na nchi za pembeni ya Ghuba ya Uajemi katika mwendelezo wa diplomasia ya ujirani hususan na nchi hizo. Ameongeza kuwa safari hiyo inalenga pia kutumia uwezo wa Iran na nchi zingine kwa ajili kustawisha uhusiano wa kisiasa na kiuchumi, hususan na Qatar.
342/